Seminari imepokea waseminari 4 wapya

Katika mwaka huu wa masomo 2018/2019, vijana wanne wa umri kati ya miaka 18 na 28 wamejiunga na Seminari ili kuanza malezi yao kuelekea Upadre. Watatu kati yao ni raia wa Tanzania (wawili kutoka DSM na mwingine kutoka Mwanza); mwingine anatoka Costa Rica (Amerika ya Kati). Pamoja na hawa, idadi ya waseminari ni 27 jumla, kutoka mataifa 12 tofauti.

Katika njia yao kuelekea Ukasisi, vijana hawa watasoma Falsafa na Theolojia, na kufanya utume wa kichungaji katika parokia za Jimbo Kuu la Dar es Salaam na katika vikundi vya makatekista vya Neokatekumenato, tayari kwa kutumwa popote duniani, Kanisa litakapowahitaji.

Miito hii mipya ya “kuacha yote na kumfuata Yesu” ni matunda ya Njia ya Neokatekumenato, ambayo ni njia ya malezi ya Kikristo kwa vijana na watu wazima iliyopo katika mataifa 134 bara zote tano, na jumuiya takriban 21300. Nchini Tanzania, Neo ipo tangu mwaka 1987, na sasa hivi inaendelea katika parokia 30 za majimbo saba: Dar es Salaam, Dodoma, Arusha, Mwanza, Morogoro, Bukoba na Tanga.