Heri ya Noeli na ya mwaka mpya 2019!

“Leo Kristo amezaliwa, leo Mwokozi ametokea;
leo malaika wanaimba duniani, malaika wakuu washangilia;
leo waadilifu wanapiga kelele kwa shangwe: Utukufu kwa Mungu juu.”

(Masifu ya Jioni ya Noeli, Antifona kwa wimbo wa Bikira Maria)

Ndugu wapendwa, imani ya Kanisa inatufundisha kuwa Noeli sio kumbukumbu tu, bali ni siku ya leo inayotekelezwa, ni ahadi inayotimizwa, ni Fumbo la Upendo linalofanyika mwili ndani ya kila mmoja wetu!

Leo Bwana anatimiza ndani mwako ahadi yake ya wokovu; leo anatuopoa kutoka machozi na kutujalia tushangilie katika Yeye kama watoto halisi, tukimpokea Mwana anayejifanya mwanadamu ili kuangamiza maovu na dhambi zetu. Leo Bwana anataka kutufanya tuwe watoto kama huyu Mtoto, wadogo kama huyu Mdogo, ili kutuingiza katika furaha ya rehema zake!

Katika siku hii takatifu, tunapenda kuwatakia wote Noeli njema kwa moyo wote, na mwaka mpya uliojaa baraka na neema tele!

Bwana wetu, aliyetoa utajiri wake ili kututajirisha na Yeye, awalipe fadhila kwa upendo na mema yote ambayo mmeonyesha kwa ajili ya Seminari na ya Uinjilishaji, na kwa kujifanya maskini kidogo ili kutusaidia katika mahitaji yetu.

Tuna furaha kubwa kutangaza, hasa kwenu ninyi mliokuwa karibu zaidi nasi miaka hii yote, kwamba baada ya siku chache, tarehe 5 Januari mwaka 2019, katika Kanisa Kuu la Dar es Salaam, watapewa daraja takatifu mashemasi wanne kutoka Seminari yetu, ambao Mungu akipenda, watapata Upadre mwezi wa saba mwakani.

Bwana awazidishie Amani yake,
Pd. Michele Tronchin, Gombera.